Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ndg. Abdul Mtaka leo Jumatano, tarehe 13 Septemba 2023 ameongoza kikao cha Kamati ya Mapato ya Wilaya iliyokaa pamoja na Wakusanya mapato wote wa Wilaya ya Rorya na Wajumbe wa BMU.
Kikao hicho kilikaa katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kufikia lengo la kukusanya mapato na kuweza kuvuka lengo walilowekewa.
Wakiongea katika kikao hicho Wakusanya mapato wametoa changamoto wanazokutana nazo katika ukusanyaji wa mapato kuwa ni pamoja na kucheleweshewa fedha za gharama ya ufuatiliaji ziwani, kucheleweshewa marejesho ya fedha za makato ya miamala wanapolipia fedha kupitia mitandao ya simu, ubovu wa barabara zinazoingia na kutoka mialoni, wavuvi kugoma kutoa ushuru wa maegesho ya mitumbwi kwa kisingizio cha kauli za kisiasa na kutokwepo kwa choo na baadhi ya Halmashauri kuomba ushuru mara mbili baada ya wateja kukata kwao na kusafirisha mazao kwenda halmashauri zingine.
Changamoto zingine ni kutopata ushirikiano wa kutosha kutoka Jeshi la Polisi hasa kwa wanaotoroka bila kulipa ushuru wa Stendi, kukosa Vitambulisho na baadhi ya Viongozi wa Halmashauri kutowatambua mbele ya Jamii wanakokusanyia ushuru ili kuwaongezea nguvu.
Mkurugenzi Mtendaji ameahidi kuwa kero zote zinazokwamisha ukusanyaji wa mapato yatatatuliwa kwa wakati na anaamini ukusanyaji wa mapato utafikia na kuvuka lengo lililowekwa kwa mwa wa fedha 2023/2024.
Wakusanyaji mapato hao wamemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa kikao hicho muhimu na wametoa pongezi zao kwa kuwajali kwa kuwalipa posho zao kwa wakati na wameahidi kuendelea kuchapa kazi ili kuletea Rorya mapato ya kutosha na kuweza kuvuka lengo.
Wajumbe wa BMU wakiongea katika kikao hicho wametoa kero zao kubwa ni pamoja na uvuvi haramu, kutekwa na kupigwa kwa Wavuvi wao wanapoenda kuvua ndani ya Ziwa Victoria na Wavuvi na Majambazi kutoka Kenya na Uganda ambapo hunyang'wa Samaki, Mazao ya Samaki na Vyombo vya uvuvi pamoja na kuuwawa. kero zingine ni kutojua kwa usahihi mipaka ndani ya Ziwa na uchakavu mkubwa wa Miundombinu ya BMU na kutorejeshewa fedha zao.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo na Mkuu wa Kitengo cha Fedha wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa BMU na kuahidi kuanza upya katika maeneo ambayo halmashauri ililegea. Hata hivyo, amesema matatizo mengine tayari yamewasilishwa katika Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mkoa na Mamlaka za Juu ya Nchi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi zaidi.
Kikao hicho kimehairishwa kwa Wajumbe wote kukubaliana kuongeza nguvu za Ukusanyaji wa Mapato na wanaamini watavuka lengo.
INGRI JUU - RORYA
Sanduku la Posta: 250 TARIME
Simu ya Mezani: 0282985583
Simu ya Mkononi :
Barua Pepe za Watumishi: mkurugenzi@roryadc.go.tz
Haki Zote Zimehifadhiwa